Rais Samia Suluhu Hassan amewataka Viongozi aliowaapisha hii leo kwenda kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha wanaleta matokeo katika kazi wanazofanya.
Rais ametoa kauli hiyo Ikulu Chamwino mkoani Dodoma wakati wa hafla ya kuwaapisha Mawaziri wanne na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kufuatia uteuzi alioufanya hapo jana.
Amewataka Viongozi hao kwenda kufanya madabdiliko katika maeneo yao kama kuna haja ya kufanya hivyo, na kamwe wasiogope kufanya mabadiliko yoyote yenye maslahi kwa Taifa.
Kwa mujibu wa Rais Samia Suluhu Hassan, mabadiliko kwa viongozi bado yanaendelea hivyo ni vema viongozi anaowateua kujituma na kufanya kazi kwa weledi.
Amesisitiza kuwa uongozi wake utazingatia matendo makali na si maneno makali, kwani maneno makali si hulka yake.
Mawaziri walioapishwa katika hafla hiyo ni Dkt. Stergomena Tax kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Ashatu Kijaji kuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, January Makamba kuwa Waziri wa Nishati, Profesa Makame Mbarawa kuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi pamoja na Dkt. Eliezer Feleshi ambaye ameapishwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.