RAIS SHEIN AFUNGA MAONESHO YA 4 YA WIKI YA VIWANDA YA SADC

0
341
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akizungumza kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam wakati akifunga Maonesho ya Nne ya wiki ya viwanda kwa Jumuiya ya maendeleo kwa nchi za Kusini mwa Afrika(SADC)

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein amefunga rasmi Maonesho ya Nne ya wiki ya Viwanda ya Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) huku akitumia nafasi hiyo kueleza kuna kila sababu ya kuifanya lugha ya Kiswahili iwe ya kuwaunganisha wanachama wa jumuiya hiyo.

Akizungumza baada ya kutembelea mabanda yaliyoko kwenye maonesho hayo pamoja na kuelezea kufurahishwa na namna ambavyo yamefana ametumia nafasi hiyo kuelezea umuhimu wa nchi za jumuiya hiyo kuendelea kusaidiana na kujengeana uwezo ili kuhakikisha wanafikia malengo ya maendeleo na hasa kupitia viwanda.

“Tunaweza kuongeza masoko na ajira kwa kupenda vya kwetu ambavyo vinazalishwa kwenye nchi za jumuiya yetu na ukweli ni chako ni chako na cha mwenzio sio chako. Hivyo umefika wakati wa kupenda bidhaa ambazo zinazalishwa na nchi wanachama wa jumuiya hiyo,”amesema Rais Shein.

Pia ametumia nafasi hiyo kueleza kuna kila sababu ya kuongeza ubora wa bidhaa ili kuvutia wanunuzi wengi zaidi na hiyo itaongeza upatikanaji wa soko la uhakika huku akisisitiza umuhimu wa nchi za SADC ni kuendelea kusaidiana kuendeleza ujuzi na maarifa na hatime kupiga hatua zaidi.

“Maonesho haya yamefana sana na nilitamani kuendelea kutembelea kila banda lakini kutokana na ratiba kubana nimelazimika kutembea kwa baadhi ya mabanda lakini ukweli washiriki wan chi zote wamejitahidi sana na muitikio ni mkubwa.Hata hivyo umefika wakati wa kutumia  Kiswahili kama kiunganishi cha mawasiliano kwa nchi za SADC, najua wapo watakaosema nakipigia debe Kiswahili lakini ukweli uliopo Kiswahili kilitumika kuwaunganisha wananchi wakati wa kukomboa nchi zetu,”amesema.

Pia amesema wananchi waliobahatika kuona maonesho hayo au waliopata taarifa kupitia vyombo vya habari anaamini kuna ujuzi ambao watakuwa wameupata na hivyo kuongeza tija ya uzalishaji wa bidhaa bora.

Hata hivyo amepata taarifa ya uwepo wa mijadala mbalimbali na kushauri mijadala hiyo itumike kutatua changamoto zilizoibuliwa ili kusonga mbele.

“Kulikuwa na mijadala ambayo ililenga kuendeleza na kuweka mikakati kuhusu kuendeleza viwanda katika nchi za SADC na kupitia mijadala hiyo naamini kuna changamoto zimeibuliwa na zimepatiwa ufumbuzi na siku hizi changamoto ni nyingi lakini kuna kila sababu ya kukabiliana nazo,”amesema.

Pia amesema ni vema mijadala hiyo ikaendelezwa kwa njia mbalimbali kwani inatoa fursa ya kupata suluhisho ya changamoto zilizopo hivyo zipatiwe ufumbuzi.

Wakati huo huo amesema Serikali zote mbili za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Zanzibar zinaendelea na mikakati ya kujenga misingi imara katika sekta ya viwanda na biashara pamoja na kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati.