Rais Samia : Tusimamie fedha za serikali

0
285

Rais Samia Suluhu Hassan amewaagiza viongozi wote kuhakikisha wanapiga vita vitendo vya rushwa na ubadhirifu katika miradi ya maendeleo ambayo inatumia fedha nyingi za serikali.

Rais Samia ametoa agizo hilo mkoani Kagera wakati wa kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, kumbukizi ya miaka 23 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kilele cha wiki ya vijana Kitaifa katika uwanja wa Kaitaba, Bukoba.

Aidha Rais Samia ameiagiza taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) pamoja na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa Zanzibar (ZAECA),
kufuatilia miradi yote ambayo haikuzingatia matumizi sahihi ya fedha ambayo imepitiwa na Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu wa 2022.

Rais Samia amekemea tabia ya viongozi kusubiri mbio za Mwenge wa Uhuru kubaini udhaifu katika miradi ya maendekeo.

Pia amewataka kujitathmini na kufanya kazi kwa weledi, wakizingatia matumizi sahihi ya fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Kwa upande wa akiba ya chakula, Rais Samia amesema kwa mwaka huu wa fedha serikali imeamua kuongeza bajeti katika sekta ya kilimo mara tatu zaidi ya ilivyokuwa mwaka wa fedha uliopita, ili kuwasaidia wakulima.

Rais Samia Suluhu Hassan amewapongeza vijana walioshiriki wiki ya vijana Kitaifa na kusema kuwa, hatua hiyo imeonyesha uthubutu wa vijana katika harakati za kuinua uchumi wao na wa Taifa.