Rais Samia Suluhu Hassan kufanya ziara Kenya

0
212

Rais Samia Suluhu Hassan tarehe 4 mwezi huu, siku ya Jumanne anatarajiwa kuanza ziara ya kikazi ya siku mbili nchini Kenya, kwa mwaliko wa Rais Uhuru Kenyatta wa nchi hiyo.

Akiwa nchini Kenya, Rais Samia Suluhu Hassan atakuwa na mazungumzo na mwenyeji wake Rais Kenyatta na kisha atalihutubia Bunge la nchi hiyo, litakalojumuisha Wabunge wa Wabunge yote mawili ya nchi hiyo.

Aidha, atahudhuria na kuhutubia mkutano wa jukwaa la Wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya utakaofanyika jijini Nairobi, kwa lengo la kujadili mambo mbalimbali yanayohusu fursa za biashara na uwekezaji zilizopo katika nchi hizo mbili.

Matukio ya ziara hiyo yatarushwa mbashara na vyombo vya habari vya redio, televisheni na mitandao ikiwemo Youtube chaneli ya Ikulu Mawasiliano na akaunti rasmi za Instagram, Facebook na Twitter

Hii ni ziara ya pili ya Rais Samia Suluhu Hassan nje ya nchi tangu aapishwe kushika wadhifa wa Urais Machi 19 mwaka huu, kufuatia kifo cha Dkt. John Magufuli aliyekuwa Rais wa Tanzania.

Ziara ya kwanza ya Rais Samia Suluhu Hassan aliifanya nchini Uganda Aprili 11 mwaka huu.