Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amempongeza Rais wa Malawi Dkt. Lazarus Chakwera katika Mkutano wa wakuu wa nchi na serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti Mpya wa Jumuiya hiyo
Katika salamu zake Rais Samia Suluhu Hassan amempongeza vile vile Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi na katibu mkuu Mtendaji Dkt. Stagomena Tax kwa kazi kubwa na nzuri ya kuiongoza Jumuiya hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita
Akihutubia katika mkutano huo wa 41 Rais Samia Saluhu Hassan ameomba ushirikiano kutoka kwa viongozi hao baada ya kuchaguliwa kuwa kinara (champion ) wa masuala ya haki za kiuchumi za wanawake katika mkutano wa Generation equality uliofanyika hivi karibuni nchini Ufaransa
Katika kukabiliana na janga la Uviko-19 Rais Samia amesema lengo la serikali yake ni kuhakikisha wananchi wote wanapata chanjo ili kuwa na kinga ya ugonjwa huo na kuziomba nchi zilizoendelea na Taasisi za kifedha za Kimataifa kuendelea kutoa misamaha au kurefusha muda wa ulipaji wa madeni kwa nchi zinazoendelea hadi pale janga hilo la Uviko-19 litakapokwisha