Rais Samia Suluhu Hassan leo amezindua Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Rasilimali Watu (Africa Heads of State Human Capital Summit) ambao uanatarajiwa kufanyika nchini Julai 25-26 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Dar es Salaam Rais Samia amesema, mkutano huo utatoa nafasi kwa wakuu wa nchi na Serikali za Afrika kujadiliana masuala mbalimbali yanayohusu rasilimali watu na maendeleo ya kiuchumi.
Amesema kuwa rasilimali watu ina mchango mkubwa katika maendeleo na kwamba Tanzania imeendelea kupiga hatua kwa kuboresha upatikanaji wa huduma za msingi ikiwemo afya, elimu, nishati, miundombinu ili kukuza mchango wao katika uchumi.
“Mbali na Afrika Kaskazini, katika nchi nyingine za Afrika viashiria vya viwango bora vya elimu vipo chini ya viwango vya dunia, upatikakaji na usimamizi wa maji bado ni changamoto, mifumo ya kisheria kudhibiti unyanyasaji kwa wanawake na watoto bado ni dhaifu,” amesema Rais akiainisha sehemu ya changamoto zinazoikumba rasilimali watu Afrika.
Awali akizungumza Waziri wa Fedha na Mipango wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba amesema utayari wa Rais Samia kuridhia Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo ni ishara ya utayari wake katika maendeleo ya rasilimali watu, si tu Tanzania bali Afrika na dunia kwa ujumla.
Baadhi ya washiriki waliotoa maoni yao kwa njia ya mtandao wameeleza kuwa mkutano huo umekuja wakati mwafaka kutokana na changamoto ambazo rasilimali watu inapitia hasa Kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo zinachangiwa na vita na migogoro ya kisiasa na kiuchumi, mabadiliko ya tabianchi na janga la UVIKO-19.