RAIS SAMIA: Panga panguaa baraza la mawaziri

0
290

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri na Katibu Mkuu Kiongozi.

Rais amemteua Balozi wa Tanzania nchini Japan, Hussein Kattanga kuwa Katibu Mkuu Kiongozi kuchukua nafasi ya Dkt. Bashiru Ally ambaye ameteuliwa kuwa mbunge.

Rais amefanya mabadiliko hayo wakati wa hafla ya kumuapisha Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango katika Ikulu ya Chamwino, mkoani Dodoma.

Akitangaza mabadiliko, Rais Samia amemteua Dkt. Mwigulu Nchemba kuwa Waziri wa Fedha na Mipango kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Dkt. Philip Mpango.

Katika mabadiliko hayo, Rais Samia amemteua Balozi Liberata Mulamula kuwa mbunge na kisha kumteua kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Rais pia amemteua Profesa Palamagamba Kabudi, aliyekuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria kuchukua nafasi ya Dkt. Mwigulu Nchemba.

Mabadiliko hayo pia yamehusisha Ofisi ya Rais TAMISEMI ambapo waziri sasa atakuwa Ummy Mwalimu akichukua nafasi ya Selemani Jafo aliyehamishiwa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira.

Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora waziri atakuwa Mohamed Mchengerwa huku George Mkuchika akibaki ofisi ya Rais kama Waziri Ofisi ya Rais, Kazi Maalumu.

Rais pia amemteua Mbarouk Nasor Mbarouk kuwa mbunge na kisha kumteua kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Mabadiliko hayo pia yameigusa Wizara ya Uwekezaji ambayo imerudishwa katika ofisi ya Waziri Mkuu na Geofrey Mwambe ameteuliwa kuwa waziri wa wizara hiyo.

Profesa Kitila Mkumbo akiteuliwa kuwa waziri wa Viwanda na Biashara.

Wateuliwa wote wanatarajiwa kuapishwa kesho Aprili 1 saa nne asubuhi Ikulu, Chamwino mkoani Dodoma.