Rais Samia : Mwalimu Nyerere alikuwa kielelezo cha uongozi bora

0
194

Watanzania wametakiwa kuendelea kuyaenzi mambo yote mazuri ambayo yalifanywa na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambrage Nyerere, ili Taifa liendelee kuwa na amani na utulivu.
 
 
Wito huo umetolewa wilayani Chato mkoani Geita na Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa kilele cha mbio maalum za Mwenye wa Uhuru, Kumbukizi ya miaka 22 ya kifo cha Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kilele cha wiki ya Vijana kitaifa.
 
Amesema Hayati Mwalimu Nyerere bado ataendelea kukumbukwa kwa kuwa kielelezo cha uongozi bora kwa Tanzania, Bara la Afrika na Duniani kote, hivyo ni muhimu kuendelea kumuenzi.
 
 
Kwa mujibu wa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa upande wa Serikali itajitahidi kufuata misingi ya haki na utawala bora wakati wote wa kutekeleza majukumu yake, ikiwa ni moja ya njia ya kuuenzi uongozi uliotukuka wa Hayati Baba wa Taifa.
  
 
Sherehe hizo za kilele cha mbio maalum za Mwenye wa Uhuru, Kumbukizi ya miaka 22 ya kifo cha Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kilele cha wiki ya Vijana kitaifa  zimehudhuriwa na wageni na Viongozi  mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa pamoja na Mjane wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, Mama Maria Nyerere.