Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani yanayofikia kilele chake Desemba Mosi mwaka huu mkoani Mbeya.
Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Juma Homera amewaambia waandishi wa habari mkoani humo kuwa maadhimisho kuelekea siku ya Ukimwi duniani yatafunguliwa tarehe 24 mwezi huu na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson katika viwanja vya Ruanda – Nzovwe jijini Mbeya.
Ameongeza kuwa, pia kutakuwa na kongamano la vijana ikiwa ni maandalizi ya kuelekekea siku ya Ukimwi duniani.
Siku ya Ukimwi duniani huadhimishwa desemba mosi ya kila mwaka ambapo Wanaharakati na Wakuu wa nchi hutumia siku hiyo kutoa elimu kuhusu namna ya kuzuia maambukizi ya virusi vinavyosababisha ukimwi, kupiga vita unyanyapaa na kuhimiza watu kwenda kufanya vipimo ili kufahamu hali zao.
Maadhimisho hayo yamekuwa yakifanyika tangu mwaka 1988.