Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) limesema linaanza kutoa rasmi gazeti maalumu ambalo litazungumzia masuala mbalimbali ya wafanyakazi nchini ambalo litafahamika kwa jina la ‘Mfanyakazi Tanzania’.
TUCTA imesema gazeti hilo linatarajiwa kuzinduliwa rasmi na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika maadhimisho ya Sherehe za Mei Mosi Kitaifa 2024 yatakayofanyika jijini Arusha.
Akizungumza na weaandishi wa habari, Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamhokya amesema gazeti hilo linamilikiwa na shirikisho hilo na kusimamiwa na Kampuni Tanzu inayoitwa Workers Development Corporation (WDC).
Amesema kuwa kipindi cha nyuma TUCTA ilikuwa na chombo chake cha habari ambacho ni gazeti lililokuwa maarufu sana na lilikuwa linaitwa Mafanyakazi.
“Hiki ndicho chombo cha habari kilichokuwa kinatumika na Vyama vya Wafanyakazi katika kutoa habari kwa wafanyakazi na umma kwa ujumla kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii, uchumi, siasa, kimataifa, burudani na michezo.
“Gazeti hili lilikuwa likitoka mara mbili kwa juma kwa siku za Jumatano na Jumamosi, lakini baadae, kutokana na changamoto za kiundeshaji, likawa linatoka mara moja kwa wiki. Lakini kuanzia mwaka 2012 gazeti hilo likashindwa kuendelea kutokana na sababu mbalimbali,” amesema Nyamhokya