Rais Samia kutunuku Kamisheni JWTZ

0
271

Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwatunuku Kamisheni maofisa wanafunzi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika Chuo cha Mafunzo wa Kijeshi (Tanzania Millitary Academy ‘TMA’) kilichopo Monduli mkoani Arusha.

Rais, anatarajiwa kuwasili Arusha hapo baadaye kwa ajili ya zoezi hilo litakalofanyika kesho Novemba 22, 2021 ikiwa ni sehemu ya ziara yake.

Mbali na Kamisheni, siku hiyo hiyo, Rais atazindua hoteli ya nyota tano ya Grand Melia iliyopo jijini Arusha.

Novemba 23, atafungua maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama shughuli itakayofanyika katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid na itakuwa mwisho wa ziara yake.

Akizungumzia ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella amesema ni neema Rais kufanya ziara mkoani humo mara mbili na kwamba jitihada zake zinaendelea kuzaa matunda hasa katika sekta ya utalii.

Aidha, amewasihi wananchi kujitokeza kwa wingi kumlaki Rais Samia wakati akitokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na pia kushiriki kwa wingi kwenye maadhimisho hayo kwani elimu itayotolewa inawahusu sana.

Katika wiki hiyo kutakuwa na utoaji wa elimu na ukaguzi madhubuti wa vyombo vya moto barabarani, katika uwanja wa maonesho wa Sheikh Amri Abeid pamoja na maeneo mbalimbali ya mkoa wa Arusha na viunga vyake.

Maadhimisho hayo kwa mwaka 2021 yamebeba kaulimbiu isemayo “Jali Maisha Yako na ya Wengine Barabarani.”