Rais Samia kutunukiwa Udaktari wa Heshima Uturuki

0
140

Chuo Kikuu cha Ankara ambacho ni cha pili kwa ukubwa nchini Utururki kinatarajiwa kumtunuku Rais Samia Suluhu Hassan Shahada ya Heshima ya Udaktari katika Uchumi ikiwa ni njia ya kutambua mchango wa uongozi wake katika kuimarisha mageuzi ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Waziri wa Mambo ya Nje Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba ameeleza kuwa mageuzi hayo nchini yameimarisha ustawi wa Tanzania, yameipatia sifa Tanzania kimataifa na kuendeleza uhusiano wa kiuchumi, kisiasa na kibiashara kati ya Tanzania na mataifa mengine ikiwemo Uturuki.

Rais Samia ambaye anaanza ziara ya kitaifa nchini Uturuki leo atatunukiwa shahada hiyo kesho mchana katika chuo hicho, hafla ambayo itaongozwa na uongozi wa chuo hicho na kuhudhuriwa na mawaziri, wanadiplomasia, wakuu wa .vitivo na wanafunzi.

Shahada hiyo itakuwa ya nne kwa Rais Samia kutunukiwa baada ya awali kutunukiwa nyingine na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru nchini India na Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA).

Baada ya hafla hiyo, Rais atapokelewa rasmi na Rais wa Uturuki, Recep Erdoğan katika Ikulu ya nchi hiyo kwa ajili ya mazungumzo rasmi na dhifa ya kitaifa.

Aidha, Rais Samia atakwenda jijini Instabul, mji mkuu wa kibiashara wa Uturuki, kwa ajili ya kongamano la kibiashara ambalo litakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na Uturuki likilenga kutangaza fursa za biashara na uwekezaji zinazopatikana Tanzania.