Rais Samia kusomesha wanafunzi 20

0
189

Rais Samia Suluhu Hassan ameahidi kuwalipia wanafunzi 20 wasio na uwezo wa kumudu gharama za masomo, ili waanze masomo ya ufundi stadi katika chuo kipya cha VETA alichokizindua leo mkoani Kagera.

Rais Samia ameyasema hayo wakati akihutubia wananchi katika eneo lilipojengwa chuo hicho cha VETA huko Burugo kata ya Nyakato, Bukoba mkoani Kagera.

Amewaagiza viongozi wa mkoa wa Kagera kutenga bajeti kwa wanafunzi watakaohitimu katika chuo hicho, ili kuwanunulia vifaa vya kuwawezesha kujiajiri mara baada ya kumaliza masomo yao.

Aidha Rais Samia amewataka viongozi wa chuo hicho cha VETA kuhakikisha miundombinu ya chuo hicho inatunzwa na kutoa hamasa kwa vijana wanaohitimu masomo yao , lengo likiwa ni kupunguza tatizo la ajira nchini.

Amemshukuru Balozi wa China nchini Chen Mingjian na Jamhuri ya watu wa China kwa msaada wa ujenzi wa chuo hicho cha VETA na kuongeza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na serikali ya China.