Rais Samia Suluhu Hassan, kesho anatarajiwa kuondoka nchini kuelekea nchini Zambia, kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais Mteule wa Taifa hilo Hakainde Hichilema.
Sherehe za kuapishwa kwa Rais huyo Mteule wa 7 wa Zambia zitafanyika katika uwanja wa Taifa wa Mashujaa jijini Lusaka.
Katika msafara wake, Rais Samia Suluhu Hassan ataongozana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Shaka Hamdu Shaka, Katibu wa Idara ya Oganaizesheni ya CCM Maudline Cyrus Castico na Waziri Mkuu Mstaafu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Mizengo Pinda.
Wengine ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM – Kombo Hassan Juma, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tanga na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM – Henry Shekifu na Mbunge wa Jimbo la Mtera na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Livingstone Lusinde.
Aidha, Rais mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Kikwete atashiriki katika sherehe hizo akiwa kiongozi wa timu ya waangalizi wa uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Zambia kutoka Jumuiya ya Madola.