Rais Samia: Jukwaa hili litaleta mabadiliko kwenye nchi za SADC

0
156

Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wajumbe wa Jukwaa la Mabunge ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC PF 53) kujadili na kupendekeza njia bora ya kukabiliana na tatizo la upungufu wa chakula katika nchi hizo.

Rais Samia amesema tafiti nyingi zimefanyika lakini hazijafanyiwa kazi na hivyo watu wanaendelea kupoteza maisha licha ya utajiri wa ardhi uliopo kwenye ukanda huo wa nchi za SADC.

Akifungua mkutano wa 53 wa Jukwaa la Mabunge ya SADC mkoani Arusha Rais Samia amesema, kumekuwa na maazimio kadhaa ambayo utekelezaji wake bado haujafikia malengo na hivyo kusababisha upungufu wa chakula miongoni mwa baadhi ya nchi katika SADC.

Amesema Tanzania imechukua hatua ya kuanzisha mpango bora wa kilimo unaojulikana kama Jenga Kesho Bora (BBT) ambao utatoa ajira kwa vijana kupitia kilimo lakini pia utaifanya Tanzania kuwa na uhakika wa chakula kupitia kilimo cha umwagiliaji.

Rais Samia ameongeza kuwa bajeti ya kilimo pia imeongezwa mara nne zaidi ambapo kwa sasa inakaribia shilingi za Tanzania Trilioni moja ili kuwezesha sekta hiyo kukua na kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula kupitia kilimo cha umwagiliaji.

Mkutano huo wa siku saba unafanyika kwa mara ya nne hapa nchini ambapo kwa mwaka huu mada kadhaa zitajadiliwa ikiwa ni pamoja na mada itakayoangazia njia za kisasa katika kilimo kama njia ya kuwa na uhakika wa chakula na ukosefu wa ajira kwa vijana.