Rais wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama (CIC), Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wapya wa jeshi aliowaapisha leo kuendelea pale waliowatangulia walipoishia.
Amesema hayo mapema leo mara baada ya kumuapisha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini Tanzania (CDF), Jenerali Jacob John Mkunda na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (C of S), Luteni Jenerali Salum Othman katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.
“Mkaanze pale General Mabeyo [Jenerali Venance Mabeyo] alipoachia. Najua kwenye jeshi hakuna mtu kuingia na yake, kama tulivyo kwenye serikali. Ukifikia, mwenzio alipoachia, unaanza hapo unakwenda mbele.”
Ametumia jukwaa hilo kumpongeza CDF aliyemaliza muda wake, Jenerali Venance Mabeyo na kueleza kwamba amelitumikia vyema jeshi, ameliacha likiwa imara, na kumtaka aendelee kuitumikia nchi katika nyadhifa atakazopangiwa.
Mabeyo aliapishwa kushika wadhifa huo Februari 2017, akipokea kijiti kutoka kwa Jenerali Davis Mwamunyange ambaye alistaafu.