Rais Samia Suluhu Hassan amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Abdel Fattah El-Sisi wa Misri, mazungumzo yaliyofanyika katika mji wa Sharm El Sheikh nchini hum.
Wakati wa mazungumzo yao, viongozi hao wamezungumzia masuala mbalimbali yanayohusu uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Misri, hasa kuwepo kwa mikakati mahsusi ya kuongeza kasi ya biashara na uwekezaji.
Pia wamezungumzia ujenzi wa mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere unaojengwa na wakandarasi kutoka Misri na kuonyesha kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi huo uliofikia asilimia 77 mpaka sasa.
Rais Samia amemueleza Rais El-Sisi kwamba Tanzania ina mpango wa kuziba njia ya kuchepusha mto na kuanza kujaza maji kwenye bwawa hilo.
Viongozi hao wawili wamesisitiza umuhimu wa kuutekeleza mradi huo kwa ubora na viwango vya uhakika hata kama utachelewa nje ya muda uliotarajiwa hapo awali.
Wamesisitiza kuwa timu ya wataalamu wa pande zote mbili wafanye kazi kwa karibu ili kutatua changamoto zinazojitokeza kwenye mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere.