Rais Samia azindua miradi ya maendeleo Kigoma

0
305

Rais Samia Suluhu Hassan amezindua hospitali ya wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma, ambayo ujenzi wake umegharimu shilingi bilioni 2.9.

Hospitali hiyo ina uwezo wa kuhudumia zaidi ya wananchi elfu mbili kwa siku.

Rais Samia Suluhu Hassan amezindua hospitali hiyo ya wilaya ya Kakonko, akiwa katika siku yake ya kwanza ya ziara yake ya siku nne mkoani Kigoma.

Rais, akiwa amefuatana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Angellah Kairuki, wametembelea na kukagua ubora wa mradi wa ujenzi wa hospitali hiyo utakaosaidia wananchi wengi wa mkoa wa Kigoma na mikoa jirani.

Aidha Rais Samia Suluhu Hassan amezindua miradi sita ya umeme katika kituo cha kupokea, kupoza na kusambaza umeme kwenda katika mikoa ya Kigoma na Geita.

Kwa upande wa miundombinu ya barabara Rais Samia amezindua barabara ya Kabingo – Nyakanazi iliyopo Kakonko Mjini na kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa barabara ya Kibondo (Mjini) – Nduta yenye urefu wa kilomita 25.9.

Rais Samia pia alitarajiwa kufanya mkutano wa hadhara katika uwanja wa Taifa wa Kibondo.