Rais Samia aweka jiwe la msingi ujenzi wa barabara Mufindi

0
165

Rais Samia Suluhu Hassan ameweka Jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya Sawala – Mkonge – Iyegeya yenye urefu wa Kilometa 40.7 inayojengwa kwa kiwango cha Lami katika wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa.

Ujenzi wa barabara hiyo unatekelezwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) chini ya mkandarasi Hematec Inverstment Ltd na G’S Contructors Co Ltd.

Rais Samia amesema katika mwaka wa fedha 2022/23 Serikali imeongeza Bajeti ya TARURA ili kujenga barabara vijijini na kuwezesha wakulima kufikisha mazao yao katika masoko kwa wakati.

Aidha, Rais Samia amepongeza amepongeza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara vijijini na Mijini (TARURA) Mhandisi Victor Seff kwa kuendelea kusimamia vizuri miradi na fedha zote zinazopelekwa katika taasisi hiyo.

Ametoa wito kwa wanachi kuendelea kulipa kodi ili kuiwezesha Serikali kuendelea kuleta fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi na kutatua kero za wananchi kwa wakati.

Akisoma taarifa ya ujenzi wa barabara hiyo Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seff, amesema Barabara hiyo ni mojawapo ya barabara zilizochaguliwa chini ya Programu ya Agriconnect awamu ya kwanza kwa Wilaya za Kilolo (km 18.3) na Mufindi (km 30.3) kwa Mkoa wa Iringa zenye jumla ya km 48.6 na Mbeya vijijini (km 26.8) na Rungwe (km 12.2) kwa Mkoa wa Mbeya km 38.4.

Kilometa 30.3 kati ya km 40.7 zimeshawekwa tabaka la lami nyepesi na usanifu wa sehemu iliyobaki ya km 10.4 unaendelea na utakamilika Mwezi Oktoba 2022. Utekelezaji wa Sehemu iliyobaki utafanyika mwaka wa fedha 2023/24.
 
Jumla ya Shilingi Bilioni 8.60 zimeshalipwa ambapo sehemu ya kwanza zimelipwa Shilingi Bilioni 4.60 na sehemu ya pili zimelipwa Shilingi Bilioni 4.6.

Mradi huu wa kimkakati una lengo kusaidia wakulima vijijini katika kuongeza/ kuimarisha Mnyororo wa thamani ya mazao yao hasa mazao ya Mbogamboga, Kahawa, Chai na mazao mengine yanayohitaji kusafirishwa kwa haraka toka Mashambani au katika maeneo ya uzalishaji hadi kufika Viwandani au katika masoko pasipo kupoteza ubora wake.