Rais Samia awataka Mawakili kusimamia haki

0
234

Rais Samia Suluhu Hassan amewataka Mawakili wa Serikali kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na uaminifu.

Amewataka Mawakili wote wa Serikali wakati wa kutekeleza majukumu yao watambue kuwa wamekabidhiwa dhamana kubwa ya sekta ya haki.

Rais Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo mkoani Dodoma wakati akifungua mkutano mkuu wa chama cha Mawakili wa Serikali ambapo pia amezindua chama cha Mawakili hao wa Serikali.

Amesema ni muhimu kwa Mawakili wa Serikali kutambua kazi ya kusimamia haki iko mikononi mwao na kwamba wananchi wengi wanahitaji msaada wa kisheria kutoka kwao.

Rais Samia amesema katika uongozi wake anatamani kuona Mawakili hao wa Serikali wanatenda haki wakati wa kuhudumia wananchi na wawasikilize pamoja na kutatua shida zao.

Kwa upande wa Serikali, Rais Samia amesema itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya sekta ya sheria wakiwemo Mawakili wa Serikali ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Pia amewapongeza kwa kuanzisha mfumo wa Mawakili wa Serikali na kuwataka Mawakili ambao hawajajisajili katika mfumo huo kufanya hivyo mara moja.