Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewasilisha salamu za pole za Rais Samia Suluhu Hassan kwa wananchi katika Kijiji cha Nditi, wilayani Nachingwea, Lindi kutokana na athari walizozipata baada ya tembo kuvamia katika vijiji vyao na kusababisha maafa kikiwemo kifo.
Waziri Mkuu amefanya ziara wilayani humo kwa ajili ya kukagua athari zilizosababishwa na uvamizi wa tembo katika mashamba ya wananchi kwenye kijiji cha Namapwiya na kuwapa pole wananchi hao.
Amesema Serikali itahakikisha hakuna mwananchi atakayekosa chakula, huku akimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea kupitia kamati ya maafa ya wilaya ahakikishe wanaandaa utaratibu wa kupatikana chakula kwa wananchi wote ambao mashamba yao yameathiriwa na wanyamapori.
Waziri Mkuu amesema tatizo hilo limechangiwa na wafugaji kuvamia maeneo ya hifadhi kwa kuingiza mifugo ikiwemo mbuzi, ng’ombe na kondoo katika hifadhi na kusababisha wanyamapori kukimbia na kwenda kwenye makazi ya wananchi.
Kufuatia hali hiyo Waziri Mkuu amemwagiza Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki kukutana na wafugaji na kuwataka kutopeleka ng’ombe na mbuzi kwenye maeneo ya hifadhi.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa wananchi kutoingia na kuendesha shughuli za kilimo katika maeneo ya hifadhi ili kuepuka mazao yao kuharibiwa na wanyamapori.
Amesema katika kuhakikisha wanyamapori wanadhibitiwa, Rais Samia ameridhia zaidi ya shilingi bilioni 1.2 zitumike kwa ajili ya ujenzi wa vituo 19 vya askari wa wanyamapori karibu na maeneo ya hifadhi.
Waziri Mkuu amesema kati ya vituo hivyo vitatu vitajengwa katika wilaya tatu za mkoa wa Lindi ambazo ni Nachingwea (Nditi), Liwale (Liwale) na Milola (Ruangwa)
Waziri Mkuu amesema Rais Samia ameridhia kibali cha ajira 6,000 za askari wa wanyamapori ambao watasambazwa katika maeneo yete yanayopakana na hifadhi ili kuendelea kuimarisha ulinzi na kudhibiti wanyamapori kuingia kwenye maeneo makazi ya wananchi.
Majaliwa amesema Serikali imetoa namba ya bure ya mawasiliano ambayo ni 0800110067 ili kuwawezesha wananchi kutoa taarifa mara wanyamapori wanapovamia kwenye makazi yao.
Akiwa katika kata ya Nditi kijiji cha Namanja kabla ya kuzungumza na wananchi Waziri Mkuu alikwenda kuifariji familia ya marehemu Riziki Issa ambaye aliuawa na tembo.
Akizungumza kwa niaba ya familia hiyo Mussa Nambole amesema wamefarijika kwa namna ambavyo viongozi mbalimbali wa Serikali walivyoshirikiana nao katika kipindi cha msiba huo.