Rais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za pole kwa ndugu, jamaa na marafiki waliopoteza wapendwa wao katika ajali ya gari iliyotokea mkoani Arusha na kusababisha vifo vya watu 25.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram pamoja na kutoa salamu za pole Rais Samia ameviagiza vyombo vya ulinzi, usalama na udhibiti kuendelea kuhakikisha vinasimamia sheria kikamilifu, ikiwemo ukaguzi wa mara kwa mara wa vyombo vya usafiri na udhibiti wa leseni kwa madereva wanaorudia kuvunja sheria mara nyingi na wakati mwingine kusababisha watu kufariki dunia.
Katika ajali hiyo iliyotokea maeneo ya Ngaramtoni Kibaoni by Pass wilayani Arumeru Februari 24, 2024, watu wengine zaidi ya 20 wamejeruhiwa.
Ajali hiyo ilihusisha lori na magari mengine madogo matatu, huku chanzo kikielezwa ni kufeli breki ya lori na kusababiaha kuyagonga magari mengine yaliyokuwa mbele yake.
Polisi mkoani Arusha wanaendelea kumtafuta dereva aliyesababisha ajali hiyo ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.