Rais Samia ana dhamira ya kufanikisha uchaguzi huru

0
263

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Abdulrahman Kinana amewahakikishia Watanzania kuwa serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kufanya uchaguzi huru na wa haki kuanzia wa Serikali za Mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Kinana ameyasema hayo mkoni Dar es Salaam alipokuwa akitoa salamu akimwakilisha Mwenyekiti wa CCM Taifa Rais Samia Suluhu Hassan katika mkutano mkuu wa chama cha ACT Wazalendo.

“Tunakwenda katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na baadaye mwakani uchaguzi mkuu. Kumefanyika mabadiliko ya sheria tatu bungeni. Sheria ya Vyama vya Siasa, Sheria ya Tume ya Uchaguzi na Sheria ya Uchaguzi. Kuna maoni yametolewa na wadau mbalimbali katika kamati za Bunge, bungeni…ukiangalia sheria ile baada ya maoni na ushauri kuna mabadiliko makubwa sana,” Amesema Kinana.

Amesema mbali na kupitisha sheria nzuri ya kuhakikisha kunakuwepo uchaguzi huru na wa haki, pia dhamira ya Rais Samia kufanikisha hilo inajipambanua katika utekelezaji wake.