Rais Samia akemea migogoro misikitini

0
121

Rais Samia Suluhu Hassan amekemea tabia ya baadhi ya viongozi wa dini ya Kiislamu kuanzisha migogoro na vurugu misikitini na badala yake amewataka wahubiri amani na upendo kwa waumini wao.

Akihutubia mara baada ya kuzindua msikiti wa Jumi’ Ul Istiqaama uliopo mkoani Kagera, Rais Samia amewataka waumini na viongozi wa dini ya Kiislamu kushikamana na kuachana na migogoro inayozorotesha ustawi wa dini hiyo.

Rais amesema, Viongozi wa taasisi nyingine za dini ya Kiislamu waige mfano wa Jumuiya ya Istiqaama ya kufanya miradi ya maendeleo yenye tija bila kuwa na mifarakano yoyote kwa ustawi wa dini na waumini wake.

“Nawaomba waislamu wenzangu, tuache mifarakano na migogoro inayosababisha kuzorotesha ustawi wa dini na badala yake tushikamane na tuwe wamoja katika kazi hii ya kumuabudu Mungu.” amesema Rais Samia

Msikiti huo wa Istiqaama uliokarabatiwa na Mfalme wa Oman umejengwa miaka 166 iliyopita na sasa umeboreshwa na kuwa wa kisasa na kuongeza uwezo wa waumini kufanyia ibada kwa mara moja kufikia watu elfu moja.