Rais Samia : Ajira wanazoweza kufanya Watanzania, wapewe

0
354

Rais Samia Suluhu Hassan ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato mkoani Dodoma na kuagiza kazi zote zinazoweza kufanywa na Watanzania wapewe wao.

Aidha, ameelekeza katika utoaji wa ajira hizo, kipaumbele kiwe kwa wananchi wanaozunguka mradi huo.

Hata hivyo, amekemea tabia ya baadhi ya wananchi ambao wanaajiriwa kwenye miradi ya Serikali na kuiba vifaa vya ujenzi, na kwamba huo ni uhujumu, na watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria.

Kuhusu mradi huo, Rais Samia Suluhu Hassan amesema ni mwendelezo wa Serikali wa kujenga viwanja vya ndege na kukarabati vilivyopo, ili kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishani na kukuza sekta nyingine zikiwemo kilimo, biashara na utalii.

Amesema mwaka huu wa fedha wanahakikisha miradi inayotekelezwa inachochea maendeleo ya watu, na kwamba wanakwenda na kauli mbiu isemayo “Tunakuza ushindani kwa ajili ya maendelelo ya watu.”

Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Msalato ambao mpango wa ujenzi ulipitishwa mwaka 1970, unajengwa kwa awamu ambapo sasa ni awamu ya kwanza inayofadhiliwa na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) kwa mkopo wa masharti nafuu wa shilingi bilioni 767.