Rais Samia aipa Taifa Stars Milioni 10

0
373

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma amesema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi Milioni 10 kwa timu ya Taifa ya soka (Taifa Stars) kufuatia goli moja walilofunga katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za AFCON mwaka 2023 dhidi ya Niger.

Mwinjuma ametoa taarifa hiyo bungeni jijini Dodoma wakati wa kipindi cha maswali na majibu, ambapo ametumia nafasi hiyo kuipongeza Stars kwa ushindi huo ulioiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu fainali hizo zitakazofanyika mwakani nchini Ivory Coast.

“… ile Milioni 10 yao ya goli la Mama wataipata leo kwa sababu mama hana kona kona, akishaahidi lazima atekeleze,” amesema Naibu Waziri.

Kufuatia ushindi huo, Stars sasa ipo nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi ikiwa na alama saba, ambapo inahitaji ushindi au sare kwenye mchezo wake wa mwisho na Algeria ili kujihakikishia nafasi kwenye mashindano hayo ambayo mara ya mwisho ilishiriki mwaka 2019 yalipofanyika Misri.