Rais wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amezindua safari za treni ya abiria kutoka Arusha kwenda Dar es Salaam na kusema kuwa usafiri huo utasaidia kutunza barabara nchini.
Katika hafla hiyo iliyofanyika jijini Arusha leo Oktoba 24, 2020, Dkt. Magufuli amesema kuwa mizigo mingi iliyokuwa ikisafirishwa kwa njia ya barabara kwenda mikoa ya Kaskazini mwa Tanzania, sasa itatumia usafiri wa treni ambao ni gharama nafuu zaidi.
Aidha, amewaasa viongozi wa serikali kujiepusha na kubinafsisha mali zenye maslahi makubwa kwa umma, kwani kabla ya ubinafsishaji, usafiri wa reli na usafiri wa anga ulikuwa ukitoa huduma kwa wananchi.
Kabla ya Rais Magufuli kuzungumza, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogo akitoa tathmini ya ukarabati huo uliofanywa na wahandisi wa ndani amesema umegharimu zaidi ya shilingi bilioni 14 ambazo zimetolewa na serikali.
Aidha, wakuu wa mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Tanga, ambayo reli hiyo imepita wamesema usafiri wa treni umesaidia usafirishaji na kukuza uchumi kwa wananchi wa maeneo hayo.
Reli hiyo ilitumika mara ya mwisho mwaka 1986.