Rais Magufuli awatakia heri Watanzania siku ya Uhuru

0
2230

Rais John Magufuli ametuma salamu kwa Watanzania wote katika kuadhimisha miaka 57 ya Uhuru wa Tanzania Bara, siku ya Jumapili Disemba Tisa.

Katika salamu zake, Rais Magufuli amewashukuru na kuwapongeza Wazee wote, wakiongozwa na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kufanikisha kupatikana kwa Uhuru wa Tanzania Bara na kwa Watanzania wote kwa kutimiza miaka hiyo 57 ya Uhuru wakiwa wamoja na nchi ikiwa na amani.

Rais Magufuli amesisitiza kuwa Disemba Tisa itakuwa ni siku ya mapumziko na kwa kwamba shilingi bilioni moja zizotengwa hapo awali kwa ajili ya maadhimisho hayo zitatumika  kujenga hospitali ya Uhuru katika Jiji la Dodoma kama ilivyotangazwa na Waziri Mkuu  Kassim Majaliwa na kuwataka Watanzania wote waitumie  siku hiyo kutafakari Uhuru uliopo, mahali walipotoka, walipo sasa na wanapoelekea.

Ameongeza kuwa amefarijika kuona katika kipindi cha miaka mitatu aliyokaa madarakani, serikali imefanikiwa kudumisha Amani, Umoja na Muungano wa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar na juhudi za kukuza uchumi zikiendelea na kuiwezesha Tanzania kuwa miongoni mwa nchi Tano ambazo uchumi wake unakua kwa kasi Barani Afrika.

Katika kuadhimisha miaka hiyo  57 ya Uhuru wa Tanzania Bara, Rais Magufuli kwa mujibu wa Mamlaka aliyopewa,  ametoa msamaha kwa wafungwa 4,477,  ambapo kati yao 1,176 watatoka siku ya maadhimisho ya  siku ya Uhuru.

Msamaha huo unawahusu wafungwa wagonjwa, wazee kuanzia miaka 70 na zaidi, wafungwa wa kike walioingia gerezani wakiwa wajawazito, na waliongia na watoto wanaonyonya au wasionyonya pamoja na wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili.

 

Halikadhalika, Rais Magufuli ameamua wafungwa waliotumikia robo ya adhabu zao, wapunguziwe robo ya adhabu zao baada ya punguzo la kawaida la theluthi moja linalotolewa kwenye Kifungu cha  49 (1) cha Sheria ya Magereza Sura ya 58.

Hata hivyo, msamaha huo hautawahusu wafungwa wanaotumikia baadhi ya adhabu zikiwemo za kunyongwa, kifungo cha maisha, biashara ya dawa za kulevya na binadamu, makosa ya unyang’anyi, kukutwa na viungo vya binadamu, makosa ya kupatikana na silaha, risasi, milipuko isivyo halali, makosa ya shambulio la aibu, kunajisi, kubaka, kulawiti na makosa  kuwapa mimba wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

Wafungwa wengine ambao hawahusiki na msamaha huo wa Rais ni wale wa makosa ya uhujumu uchumi, rushwa, ubadhirifu, ujangili, waliowahi kupunguziwa kifungo kwa msamaha wa Rais, wanaotumikia kifungo chini ya Sheria ya Bodi ya Parole, wenye makosa ya kutoroka au kujaribu ama kusaidia kutoroka chini ya ulinzi halali, walioingia gerezani baada ya Disemba Mosi mwaka huu  au waliowahi kufungwa na kurudi tena gerezani pamoja na wenye makosa ya kinadhamu magerezani.