Rais Magufuli awataka madereva kuzingatia sheria

0
554

Rais Dkt. John Magufuli amewataka madereva wanaoendesha vyombo vya usafiri wa abiria kuzingatia sheria na taratibu za usalama barabarani wakati wote wa safari zao.

Rais Magufuli amesema hayo leo katika Kijiji cha Kihanga, Wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera alipokutana na abiria na dereva wa basi dogo linalofanya safari zake kati ya Bukoba na Karagwe.

Amesema ajali nyingi za barabarani husababishwa na ukiukwaji wa sheria na taratibu za usalama barabarani na kwamba jukumu la kuhakikisha sheria na taratibu hizo zinatekelezwa lipo mikononi mwa watumiaji wote wa barabara hasa madereva wanaoendesha vyombo vya usafiri.

Kwa baadhi ya abiria hao ambao ni wanafunzi, Rais Magufuli amewataka kusoma kwa bidii na kufanya vizuri katika masomo yao.

Baadhi ya wananchi waliopata fursa ya kukutana na Rais Magufuli wakaonyesha furaha yao.

Rais Magufuli yuko mapumzikoni Wilayani Karagwe katika Mkoa wa Kagera.