Rais Magufuli awasamehe wafungwa 3900 kuelekea sikukuu ya muungano

0
750

Rais Dkt. Magufuli amewatakia heri Watanzania wote katika kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 56 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ambapo pia ametangaza msahama kwa wafungwa 3,973.

Kati ya wafungwa hao, wafungwa 3,717 wamesamehewa vifungo vyao, na wafungwa 256 waliokuwa wanakabiliwa na adhabu ya kunyongwa hadi kufa wamebadilishiwa adhabu hiyo.

Rais Magufuli amesema ana matumaini kuwa wafungwa hao wamejifunza na watajirekebisha ili waungane na jamii katika kulitumikia Taifa wakiwa raia wema wanaozingatia sheria na taratibu.

Pamoja na hilo Rais Magufuli amewataka Watanzania wote kutumia siku ya kesho (26 Aprili, 2020) kuutafakari Muungano ulioasisiwa na viongozi wakuu Baba wa Taifa, Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Hayati Sheikh Abeid Amani Karume pamoja na kumuomba Mwenyezi Mungu aepushe janga la ugonjwa wa Corona.

Aidha, Rais Magufuli amewakumbusha Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Corona (Covid-19) ikiwemo kujiepusha na mikusanyiko na safari zisizo za lazima.