Rais Magufuli ateta na Waziri Mkuu wa India

0
245

Waziri Mkuu wa Narendra Modi amempigia simu Rais John Magufuli ambapo viongozi hao wamezungumzia masuala yahusuyo uhusiano na ushirikiano mzuri wa kirafiki na kihistoria uliopo kati ya Tanzania na India.

Katika mazungumzo hayo Modi amempongeza Rais Magufuli kwa uongozi wake mahiri na amemtakia heri yeye na Watanzania wote katika juhudi kubwa za kuijenga nchi zinazoendelea na uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.

Pamoja na kumhakikishia kuwa India itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano wake na Tanzania katika nyanja mbalimbali hasa kiuchumi, Modi amempa mrejesho wa yaliyojiri katika mkutano wa nchi 20 tajiri duniani (G20) uliofanyika hivi karibuni ambapo nchi hizo zimekubaliana kuwa taasisi za fedha za kimataifa zitoe msamaha wa madeni kwa nchi masikini na zinazoendelea, zilizopata madhara kutokana ugonjwa wa corona

Rais Magufuli amemshukuru Waziri Mkuu Modi kwa kumpigia simu, kumtakia heri na kumpa mrejesho wa yaliyojiri katika mkutano wa G20, na ameomba taasisi za fedha za kimataifa zitakapotoa msamaha wa madeni ziitupie macho Tanzania ambayo pia imepatwa na madhara ya ugonjwa wa corona ili iweze kuimarisha uchumi wake.

Aidha, Rais Magufuli ameipongeza India kwa juhudi za kutafuta chanjo ya virusi ya corona ambazo anaamini zitafanikiwa na kwamba Tanzania ikiwa moja ya nchi zilizokubwa na ugonjwa huo itanufaika, japo ugonjwa wenyewe unapungua kwa kasi kubwa nchini.

Rais Magufuli amemshukuru Modi kwa uhusiano na ushirikiano mzuri wa Tanzania na India ambayo ni miongoni mwa nchi tano  zinazoongoza kwa uwekezaji hapa nchini na pia ameshukuru kwa mikopo nafuu inayotolewa na India kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa hapa nchini.

Ameitaja baadhi yake kuwa ni mkopo wa ujenzi wa Taasisi ya Teknolojia ya Nelson Mandela, mikopo ya miradi ya maji na ufadhili wa masomo ya elimu ya juu kwa wanafunzi wa Tanzania wanaokwenda kusomea masuala ya afya, uhandisi na TEHAMA nchini India.