Rais Magufuli ateta na Wadau wa madini

0
1036

Rais John Magufuli amesema kuwa  yupo tayari kupeleka hati ya dharura katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kufanya mabadiliko ya kodi mbalimbali wanazotozwa wafanyabiashara wa madini,  endapo wafanyabiashara hao watatoa mapendekezo yatakayosaidia kuongeza makusanyo katika sekta hiyo.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo jijini Dar es salaam wakati akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini, wafanyabiashara na wadau wa sekta ya madini, mkutano uliokuwa na lengo ya kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili wachimbaji hao na namna ya kuzitatua.

Ametoa kauli hiyo baada ya wafanyabiashara hao wa madini kulalamika kuwa kumekuwa na kodi nyingi katika biashara ya madini,  jambo linalosababisha baadhi yao kukwepa kodi.

Awali wakati wa mkutano huo, Rais Magufuli alitoa nafasi kwa wachimbaji, wafanyabiashara na wadau mbalimbali waliohudhuria mkutano huo  kutaja changamoto zinazowakabili ambapo alitumia takribani saa sita kusikiliza changamoto hizo.

Wakitaja changamoto zao, baadhi ya Wadau hao wa sekta ya madini nchini  wameishauri serikali  kuondoa kodi mbalimbali ambazo zimekua zikiwaumiza wachimbaji wadogo wa madini ikiwa ni pamoja na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Mkutano huo unaoshirikisha wachimbaji wadogo wa madini, wafanyabiashara na wadau wa sekta ya madini, utaendelea Jumatano Januari 23 mwaka huu  ambapo yanatarajiwa kufanyika majadiliano mbalimbali yenye lengo la kuboresha sekta ya madini nchini.