Rais Dkt. JOHN MAGUFULI amefanya ziara ya kushtukiza katika mradi wa ujenzi wa daraja linalokatiza baharini kuunganisha eneo la AGA KHAN na UFUKWE WA COCO jijini DSM kujionea maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo.
Katika ziara hiyo Rais Dkt. MAGUFULI ameshuhudia kazi ya ujenzi ikiendelea vizuri ambapo mkandarasi ambaye ni Kampuni ya GS Engineering ya KOREA anakamilisha kuunganisha daraja la muda litakalomwezesha kuanza ujenzi wa nguzo za daraja.
Akiwa katika mradi huo, Rais Dkt. MAGUFULI amekutana na mhandisi mshauri kutoka kampuni ya YOOSHIN, Mhandisi SUK-JOO LEE na kumuelezea kufurahishwa na maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo.
Daraja hilo ambalo linatarajiwa kukamilika Oktoba 2021, litakuwa na urefu wa kilomita 1.03 na barabara za kuunganisha zenye urefu wa kilomita 6.23 na kugharimu takriban shilingi bilioni 255.
Kwa sasa ujenzi wa daraja hilo linalopendekezwa kuitwa TANZANITE, umefikia asilimia 10.12.