Rais Dkt. John Pombe Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa familia, Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma na Waumini wa Kanisa la Anglikana kufuatia kifo cha Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhani kilichotokea leo asubuhi tarehe 28 Aprili, 2020 jijini Dar es Salaam.
Rais Magufuli amesema marehemu Jaji Mkuu Mstaafu Augustino Ramadhani atakumbukwa kwa utumishi uliotukuka kwa nchi yake, ulioshadidishwa na umahiri wake, ukweli, uchapakazi, uzalendo wakweli, na ucha Mungu.
“Nakumbuka nilipokwenda kumuona hospitali mazungumzo yake yalikuwa ni ya kumtumaini na kumtegemea Mungu, kwa hiyo na mimi namuombea kwa Mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi, Amina,” amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli amempa pole Jaji Mkuu wa Tanzania na amemuomba kufikisha salamu zake za pole kwa familia ya marehemu, majaji, mahakimu na wafanyakazi wote wa mahakama pamoja na waumini wa Kanisa la Anglikana kwa kuondokewa na mpendwa wao.
Raha ya milele umpe ee Bwana, na mwanga wa milele umuangazie, Marehemu Augustino Ramadhani astarehe kwa amani, Amina.