Rais Magufuli amuapisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali

0
272

Takribani wiki moja baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Tanzania, Dkt. John Magufuli ameanza kupanga safu ya uongozi wake ambapo leo Novemba 9, 2010 amemuapisha Prof. Adelardus Kilangi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kipindi cha pili.

Katika hafla hiyo iliyofanyika Ikulu, Chamwino jijini Dodoma, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma, Spika Job Ndugai na Katibu Mkuu Kiongozi, John Kijazi, Prof. Kilangi amemshukuru Rais Dkt. Magufuli kwa kumuamini kwa mara ya pili na kumuahidi kwamba atatumika kwa nguvu na uwezo wake wote.

“Ninaahidi kufanya kazi kwa akili yangu yote, nguvu zangu zote, kwa uwezo wangu wote na nikishirikiana na watumishi wa serikali katika kutatua changamoto,” amesema Kilangi.

Akizungumzia kazi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, nafasi ambayo ameitumikia kwa miaka miwili sasa tangu alipoteuliwa mara ya kwanza mwaka Februari 2018, Kilangi amesema sio lazima awe mtu aliyebobea sana kwenye sheria, bali anapaswa kuwa mtu anayetambua muktadha ambao sheria zitatumika.

Aidha, Rais Dkt. Magufuli pamoja na baadhi ya viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo wamempongeza Prof. Kilangi kwa kuteuliwa na kumtakia kila ka heri katika utumishi wake.

Dkt. Magufuli alimteua Dkt. Kilangi kushika wadhifa huo Novemba 5 mwaka huu baada ya kipindi chake cha kwanza kumalizika siku hiyo hiyo.