Rais, Dkt. John Magufuli ametoa siku 53 kwa mkandarasi anayetekeleza mradi wa Ujenzi wa Kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo mikoani na nje ya Nchi cha Mbezi Luis, Dar es Salaam kuwa amekamilisha kazi hiyo.
Dkt. Magufuli ametoa agizo hilo katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi katika mradi huo aliyoifanya akiwa na Rais wa Malawi, Dkt. Razarus Chakwera na kusisitiza kuwa kabla ya Novemba 30 mradi huo uwe umekamilika.
Aidha, Dkt. Magufuli amemtaka mkurugenzi wa jiji la Dar es Salaam kuhakikisha ujenzi unashika kasi na kukamilika mapema iwezekanavyo.
“Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam wewe ndio ulisaini ujenzi wa mradi huu, siridhishwi na kasi ya ujenzi, nataka mradi huu ukamilike mwezi Novemba, mfanye kazi usiku na mchana.”
Kwa upande wake Rais wa Malawi, Dkt. Chakwera amesema umuhimu wa mradi huu si tu kwa Tanzania bali katika ukanda wote wa nchi za SADC.
“Tanzania ni mfano na inaonesha njia kwa kutumia fedha za ndani, ni wakati muafaka kwa nchi za Afrika kujisemea zenyewe na kuungana pamoja kufikia maendeleo makubwa ya kiuchumi,” Dkt. Chakwera ameongeza.