Rais Magufuli akabidhiwa mfumo wa TTMS

0
1292

Rais Dkt. John Magufuli amekabidhiwa mfumo mpya wa kusimamia uwazi katika mawasiliano ya simu – TTMS na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania –TCRA huku akiwataka watanzania kutumia vema sekta ya mawasiliano.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika jijini DSM Rais Magufuli amesema mfumo huo una manufaa kwa taifa na kuwataka TCRA kuulinda kwa nguvu zote kwa kuwa ni nyeti.

Rais Magufuli ametoa agizo kwa watanzania kuhakikisha wanatumia vema mitandao kwani imesababisha madhara makubwa duniani ikiwemo uhalifu wa kimtandao na uvunjwaji na mmomonyoko wa maadili.

“Naomba TCRA mhakikishe mnatoa adhabu kali kwa wananchi wanaotumia vibaya mawasiliano kwani hawa wanachangia kuleta maafa hapa nchini”alisema Rais Magufuli.

Mfumo huo ulianza kutumika mwaka 2013 ambapo mpaka sasa umeongeza faida nchini ikiwemo kuongeza mapato kutokana na kodi inayopatikana kwenye kampuni za simu ambapo shilingi Bilioni 93 zimepatikana.

Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Isack Kamwelwe amesema mfumo huo mpya umewezesha kutambua masuala mbalimbali ikiwemo mawasiliano ya simu yanayofanyika kwa udanganyifu na mifumo ya  simu za udanganyifu iliyokuwa imeunganishwa.