Rais Magufuli aikabidhi rungu wizara ya maji

0
233

Watendaji wa wizara ya maji wametakiwa kushirikiana na kuchapa kazi kwa umoja ili kukamilisha miradi iliyokuwa imeanzishwa na kukwama.

Hayo yamesemwa na Rais Dkt. John Magufuli mara baada ya kuzindua mradi wa upanuzi wa mtandao wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda katika miji ya ya Kagongwa na Isaka mkoani Shinyanga.

Aidha, Rais Magufuli amewapongeza watendaji wa wizara ya maji kwa namna walivyoanza kusimamia utekezaji wa miradi mbalimbali hapa nchini na kuwaambia wasisite kuwachukulia hatua watendaji wanaokwamisha miradi hiyo

“Waziri umeanza vizuri sana katika kuhakikisha maji yanapatikana kwa wananchi, hivyo kwa wale wanaohusika kujenga miradi na wanakwamisha nakuagiza wafukuze kabla sijakufukuza wewe na majina yao wale wote ambao ni wababaishaji yapelekwe katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ili watambulike hivyo,” ameeleza Dkt. Magufuli

Kwa upande wake Waziri wa Maji, Juma Aweso ameahidi yeye na watendaji wenzake katika wizara hiyo kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha lengo la kumtua mama ndoo kichwani linatimia

“Niahidi kuwa sisi kama watendaji hatutalala ni kazi usiku na mchana kuhakikisha miradi iliyokuwa ikisuasua, hii tunaiita miradi kichefuchefu na tumejipanga kukabiliana na kila kikwazo cha miradi hiyo ila Watanzania wafurahie huduma maji,” ameeleza Waziri Aweso

Mradi wa upanuzi wa mtandao wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda katika miji ya Kagongwa na Isaka ulitengewa bilioni 24, zimetumika bilioni 23 ambaopo kiasi kilichobaki Rais Magufuli ameagiza kitumike kusambaza maji kwa wakazi wanaouzunguka mradi huo kuanzia leo.