Rais Magufuli aifagilia TAKUKURU

0
293

Rais John Magufuli ameupongeza uongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) kwa kazi nzuri ya kupambana na vitendo vya rushwa katika maeneo mbalimbali nchini.


Rais Magufuli ametoa pongezi hizo Ikulu jijini Dar es salaam wakati akipokea taarifa ya utendaji kazi ya TAKUKURU kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo Diwani Athumani, tukio lililofanyika pamoja na lile la kumuapisha Balozi wa Tanzania nchini CUBA, – Valentino Mlowola.


Amesema kuwa katika siku za hivi karibuni TAKUKURU imeweza kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wakubwa wa rushwa na hata wafanyakazi wa TAKUKURU waliokua wakijihusisha na vitendo vya rushwa, jambo linalotakiwa kupongezwa.


Rais Magufuli amesisitiza kuwa rushwa bado ipo nchini, hivyo ni vema mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa yakaendelezwa kwa kushirikisha taasisi na wadau mbalimbali.


Kwa upande wa Balozi mpya wa Tanzania nchini Cuba, -Valentino Mlowola, Rais Magufuli amemtaka kwenda kusimamia maslahi ya Taifa na kuhakikisha uhusiano baina ya nchi hizo Mbili unaimarishwa.


Tukio la uwasilishaji wa taarifa ya utendaji kazi ya TAKUKURU pamoja na lile la kumuapisha Balozi wa Tanzania nchini CUBA, – Valentino Mlowola limehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahimu Juma.