Rais Dkt. John Magufuli amemteua Dkt. Islam Seif Salum Mchenga kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu (Deep Sea Fishing Authority – DSFA) na kumteua Dkt. Emmanuel Sweke kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi imeeleza kuwa uteuzi wa viongozi hao umeanza tarehe 01 Desemba, 2018 ambapo kabla ya uteuzi huo Dkt. Islam Seif Salum Mchenga alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi – Zanzibar huku Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Dkt. Emmanuel Sweke kabla ya uteuzi huu alikuwa Afisa Utafiti wa Uvuvi Mwandamizi na Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Uvuvi Tanzania (Tanzania Livestock Research Institute – TAFIRI) – Kigoma.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amemteua Prof. Sebastian Chenyambuga kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI) na kumteua Prof. Justinian Ikingura kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (Geological Survey of Tanzania – GST).
Uteuzi wa Prof. Chenyambuga umeanza tarehe 26 Januari, 2019 huku Uteuzi wa Prof. Ikingura umeanza tarehe 18 Januari, 2019.