Rais Magufuli afanya mabadiliko ya wakuu wa mikoa na wilaya

0
330

Rais John Magufuli leo Julai 17, 2020 amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali kama ifuatavyo;

Kwanza, Rais Magufuli amemteua Dkt. Jumanne Fhika kuwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe. Kabla ya uteuzi huo, Dkt. Fhika alikuwa Ofisi ya Rais na anachukua nafasi ya Christopher Ole Sendeka.

Pili, Rais Magufuli amemteua Dkt. Aloyce Nzuki kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii. Kabla ya uteuzi huo, Dkt. Nzuki alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii na anachukua nafasi ya Prof. Adolf Mkenda.

Tatu, Rais Magufuli amemteua Mhandisi Anthony Sanga kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji. Kabla ya uteuzi huo, Mhandisi Sanga alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na anachukua nafasi ya Prof. Kitila Mkumbo.

Nne, Rais Magufuli amemteua Dkt. Allan Kijazi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii. Dkt. Kijazi anachukua nafasi ya Dkt. Aloyce Nzuki aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, na pia Dkt. Allan Kijazi ataendelea kuwa Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).

Tano, Rais Magufuli amemteua Mhandisi Nadhifa Kemikimba kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji. Kabla ya uteuzi huo, Mhandisi Kemikimba alikuwa Mkurugenzi katika Wizara ya Maji na anachukua nafasi ya Mhandisi Anthony Sanga ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji.

Sita, Rais Magufuli amemteua Fadhili Juma kuwa Mkuu wa Wilaya ya Geita Mkoani Geita. Kabla ya uteuzi huo, Juma alikuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Lindi na anachukua nafasi ya Josephat Maganga ambaye amehamishwa kituo cha kazi na kuwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma. Maganga anachukua nafasi ya Patrobas Katambi.

Wateule wote wawepo Ikulu, Chamwino Mkoani Dodoma Julai 20, 2020 saa 4:00 asubuhi.