Rais John Magufuli ameelezea kutoridhishwa na utendaji kazi wa mkandarasi Nyanza Road Works anayejenga barabara ya Bulamba-Kisorya iliyopo mkoani Mara.
Rais Magufuli ameyasema hayo wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa barabara hiyo na kuiagiza wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuhakikisha mkandarasi huyo anafanya kila linalowezekana ili ujenzi wa barabara hiyo ukamilike katika muda wa nyongeza ambao ni miezi 35.
Barabara hiyo ya Bulamba – Kisorya ina urefu wa Kilomita 51 na imeanza kujengwa mwaka 2014 kwa gharama ya zaidi ya shilingi Bilioni hamsini.
Kabla ya Rais Magufuli kuweka jiwe hilo la msingi la ujenzi wa barabara hiyo ya Bulamba – Kisorya iliyoko mkoani Mara, alizindua kiwanda cha Lakairo Industries Group Limited kilichopo wilayani Magu.
Akizungumza na wafanyakazi wa kiwanda hicho pamoja na wananchi waliojitokeza kumlaki, Rais Magufuli ameiagiza wizara za Fedha na Mipango na ile ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kuwawezesha wawekezaji wazawa ili washiriki vizuri katika kuimarisha uchumi wa nchi.
Rais Magufuli pia alielekea wilayani Ukerewe ikiwa ni sehemu ya ziara yake mkoani Mwanza, ambapo amezindua mradi wa upanuzi wa chuo cha ualimu cha Murutunguru na mradi wa maji katika kijiji cha Nebuye wilayani humo.