Rais Magufuli aahidi kuboresha maslahi wa watumishi wa afya

0
428

Rais Dkt. John Magufuli ameahidi kuwa serikali yake itaboresha maslahi ya watumishi wa afya, huku akiwataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii kwa kitanguliza uzalendo wa Taifa mbele.

Dkt. Magufuli amesema hayo wakati akizungumza na wananchi pamoja na watumishi wa afya mara baada ya kuweka wa jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la magonjwa ya dharura katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora-Kitete.


Jengo la magonjwa ya dharura katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora-Kitete.

Ametoa ahadi hiyo mara baada ya kupewa taarifa kuwa kuna madaktari wameondoka licha ya kupangiwa kazi hospitalini hapo kwa madai kuwa hawajaridhika na kiwango mishahara.

“Hakuna mtu anayeridhika na mshahara, hata mimi siridhiki nao, hata manesi hawa hawaridhiki lakini wanajituma. Tunataka sisi wote matatizo yetu tuyatatue kwa pamoja. Hatuwezi tukayatatua kwa siku moja halafu mtu akaingia kwa selfishness [ubinafsi],” Dkt. Magufulia amewaeleza wananchi waliokuwa wakimsikiliza.

Amesema kwa miaka mitano iliyopita tayari serikali imeanza kuchukua hatua kadhaa kuboresha sekta ya afya ikiwa ni pamoja na kuajiri watumishi zaidi ya 14,000 na kujenga hospitali za rufaa na mikoa, wilaya na vituo vya afya vipatavyo 1,198.


Jengo la magonjwa ya dharura katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora-Kitete.

“Tumeanza na hivi, baadaye tunaingia kwenye maslahi ya mtumishi wa afya, tunajua wanafanya kazi kubwa sana ya kujitolea,” amesema Dkt. Magufuli huku akiwasihi watumishi wa sekta hiyo kuwa wazalendo kwani mtumishi anapokimbia anawaacha wananchi wanaohitaji huduma wakiteseka.

Wakati huo huo, amemuagiza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima kufuatilia madaktari waliokimbia vituo vya kazi na kwamba ikiwezekana daktari na hospitali zilizowachukua zifungiwe.