Rais Katalin: Ushirikiano wa Hungary na Tanzania una manufaa

0
259

Rais wa Hungary, Katalin Novák amesema ushirikiano baina ya nchi yake na Tanzania umekuwa na manufaa makubwa kutokana na kila nchi kushirikiana na nyingine katika maendeleo.

Akizungumza mara baada ya mazungumzo yake na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Rais Katalin amesema manufaa yanayoonekana moja kwa moja ni pamoja na ya sekta ya elimu ambapo nchi hizo mbili zitakuwa na uwezo wa kubadilisha wanafunzi na ujuzi.

Amesema kuwa nchi yake ipo tayari kuendelea kushirikiana na Tanzania katika mambo mbalimbali hasa yanayohusu uongozi na kuwawezesha wanawake kiuchumi na katika uongozi.

Rais huyo amemualika Rais Samia kutembelea nchini kwake ili kujionea maendeleo yaliyofikiwa na taifa hilo mwanachama wa Jumuiya ya Ulaya.

Amesema kwa sasa nchi hiyo inakabiliwa na wimbi la wakimbizi kutoka nchini Ukraine ambapo zaidi ya wakimbizi milioni mbili wamekimbilia Hungary na hivyo kuwa na mzigo mkubwa wa kuwahudumia.