Rais ataka riba za mikopo kupunguzwa

0
158

Rais Samia Suluhu Hassan leo amefungua jengo la Benki Kuu ya Tanzania Tawi la Mwanza, ambapo ametumia nafasi hiyo kuipongeza BoT kwa usimamizi wa sekta ya fedha nchini.

Rais ametaja mafanikio mbalimbali ambayo BoT imeyapata ikiwa ni pamoja na kuimarisha uchumi ambapo katika kipindi cha miaka 5 iliyopita uchumi wetu umekuwa kwa wastani wa asilimia 6.2 na kudhibiti mfumuko wa bei kwa asilimia 4.2.

Mbali na hayo, ameitaka benki kuu kuangalia masharti na riba zinazotolewa na Benki na taasisi za fedha nchini kwani wananchi wengi wanashindwa kukopa kwenye benki na taasisi nyingine za fedha kutokana na masharti ya kukopa kuwa magumu na viwango vya riba kuwa juu.

Amezitaka benki na taasisi za fedha kutengeneza mazingira mazuri kwa kutoa mikopo ya muda mrefu kwani benki nyingi na taasisi za fedha hutoa mikopo ya muda mfupi na hivyo kusababisha wananchi kushindwa kukopa.

Aidha, ameiagiza BOT kufanya maandalizi kuhusu matumizi ya sarafu za kimtandao, ili mabadiliko hayo yatakapofika nchini, yasiikute nchi haijajiandaa.

“Tumeshuhudia kuibuka kwa safaru mpya kwa njia ya kimtandao, yaani cryptocurrency. Najua bado nchini ikiwemo Tanzania hazijakubali au kuanza kuzitumia safaru hizo. Hata hivyo, wito wangu kwa Benki Kuu ni vyema mkaanza kufanyia kazi maendeleo hayo. Yakija yakitukamata, yasitukamate hatuko tayari,” ameeleza Rais Samia Suluhu Hassan

Kesho tarehe 14 Juni, 2021, Rais Samia Suluhu Hassan ataendelea na ziara yake mkoani Mwanza kwa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Reli ya kisasa yani (SGR) kipande cha tano kutoka Mwanza hadi bandari ya nchi kavu Isaka mkoani Shinyanga, atafanya ukaguzi wa Ujenzi wa daraja la JPM pamoja na ufunguzi wa Mradi wa Maji Misungwi.