DODOMA: Rais Samia Suluhu Hassan leo Julai 1, 2021 amepokea Taarifa ya Ukaguzi Maalum kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), inayohusu matumizi ya fedha zilizotolewa Benki Kuu ya Tanzania (BT) kati ya mwezi Januari na Machi mwaka huu.
Taarifa hiyo inatokana na agizo alilolitoa Rais Samia tarehe 28 Machi 2021, wakati akipokea Taarifa ya CAG kwa mwaka 2019/ 2020.
Katika taarifa ya ukaguzi maalum, CAG Charles Kichere amesema katika ukaguzi uliofanyika imebainika kuwa fedha zilizotolewa BoT katika kipindi hicho zilifuata taratibu zote, isipokuwa baadhi ya malipo yaliyokuwa yanatoka Hazina Kuu kwenda katika Taasisi mbalimbali za Serikali yalibainika kuwa na mapungufu.
Mapungufu hayo ni pamoja na baadhi ya taasisi kama vile Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), kufanya malipo mara mbili kwa kazi moja au kuchelewa kutumia fedha zilizoidhinishwa kwa ajili ya malipo ya kazi husika.
Vilevile, CAG Kichere amesema yamejitokeza mapungufu ambapo baadhi ya Makandarasi waliotoa huduma kucheleweshewa malipo yao hali inayosababisha madeni ya makandarasi kuwa makubwa kutokana na riba ambayo ni mzigo kwa Serikali.
Mapungufu mengine ni pamoja na kuwepo kwa miradi ambayo haikupangwa na hivyo kufanya malipo nje ya bajeti ya Serikali.