Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za pole kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Venance Mabeyo, kufuatia kifo cha Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Elias Kwandikwa kilichotokea tarehe 02 Agosti, 2021 Jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa ya kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, Rais amesema amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Waziri Kwandikwa ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Ushetu mkoani Shinyanga kutokana na mchango wake mkubwa katika utumishi wa umma.
“Tumempoteza mtu muhimu ambaye mchango wake katika utumishi wa umma hautasahaulika, Kwandikwa alikuwa kiongozi shupavu ambaye alikuwa akitekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria na taratibu”- Amesema Rais Samia Suluhu Hassan.
Rais amemtaka Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Mabeyo kufikisha salamu zake za pole kwa familia ya Marehemu, ndugu, jamaa, marafiki na watu wote walioguswa na msiba huo.