Rais afurahishwa na Airtel kuongeza hisa za Serikali

0
327

Rais John Magufuli amesema amefurahishwa na hatua na iliyofikiwa Kampuni ya Bharti Airtel ya kuongeza hisa zinazomilikiwa na Serikali ya Tanzania katika Kampuni ya Airtel Tanzania kutoka Asilimia 40 hadi Asilimia 49 na hivyo kupunguza hisa zilizokuwa zikimilikiwa na Bharti Airtel.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo baada ya kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Kampuni ya Bharti Airtel, Sunil Mittal, Ikulu Jijini Dar es salaam ambapo wamezungumzia maendeleo ya mazungumzo ya umiliki wa hisa za kampuni ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kampuni ya Bharti Airtel, Sunil Mittal ameongeza kuwa mazungumzo kati ya kampuni yake na Serikali ya Tanzania yanakwenda vizuri na kwamba kampuni ya Bharti Airtel imeridhishwa na makubaliano yaliyofikiwa katika masuala yaliyokuwa yakijadiliwa yenye lengo la kuiimarisha kampuni ya Airtel, kuleta manufaa kwa pande zote mbili na kuboresha huduma za mawasiliano za kampuni hiyo.