Rais afanya uteuzi wa wakuu wa mikoa

0
518
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumza na Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam Mei 7, 2021 katika Mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Mlimani City mkoani Dar es Salaam.

Rais Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa wakuu wa mikoa wapya, wengine amewabadilisha vituo vya kazi, huku wawili.wakisalia katika vituo vyao vya awali.

Katika uteuzi huo Anthony Mtaka ameteuliwa kuwa mkuu wa mkoa wa Dodoma, na kabla ya uteuzi huo alikuwa mkuu wa mkoa wa Simiyu.

Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Zainab Telack kuwa mkuu wa mkoa wa Lindi ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa mkuu wa mkoa wa Shinyanga na anachukua nafasi ya Godfrey Zambi ambaye amestaafu.

Amemteua Mhandisi Robert Gabriel kuwa mkuu wa mkoa wa Mara na kabla ya uteuzi huo alikuwa mkuu wa mkoa wa Geita.

Juma Homera ameteuliwa kuwa mkuu wa mkoa wa Mbeya na kabla ya uteuzi huo alikuwa mkuu wa mkoa wa Katavi.

Rais Samia Suluhu Hassan ameteuliwa Martin Shigella kuwa mkuu wa mkoa wa Morogoro ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa mkuu wa mkoa wa Tanga na anachukua nafasi ya Loata Ole Sanare ambaye amemaliza muda wake.

Brigedia Jenerali Marco Gaguti ameteuliwa kuwa mkuu wa mkoa wa Mtwara na kabla ya uteuzi huo alikuwa mkuu wa mkoa wa Kagera na anachukua nafasi ya Gelasius Byakanwa ambaye atapangiwa majukumu mengine.

Albert Chalamila ameteuliwa kuwa Mkuu wa mkoa wa Mwanza na kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya.

Rais amemteua Aboubakar Kunenge kuwa mkuu wa Mkoa wa Pwani na kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na anachukua nafasi ya Mhandisi Evaristv Ndikilo ambaye amestaafu.

Joseph Mkirikiti ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara na anachukua nafasi ya Joachim Wangabo ambaye amestaafu.

Dkt. Binilith Mahenge ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Singida na Kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na anachukua nafasi ya Dkt. Rehema Nchimbi ambaye amestaafu.

Dkt. Philemon Sengati ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga na Kabla ya uteuzi huo Dkt. Sengati alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, John Mongella ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na Ally Hapi sasa anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora akitokea mkoa wa Iringa.

Rais Samia Suluhu Hassa pia amemteua Adam Malima kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara,
David Kafulila anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha kuchukua nafasi ya Idd Kimanta ambaye amestaafu na Amos Makalla ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.l kuchukua nafasi ya Aboubakar Kunenge ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani.

Rosemary Staki Senyamule ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita kuchukua nafasi ya Robert Gabriel ambaye anaenda mkoani Mara, Queen Sendiga anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa na Meja Jenerali Charles Mbuge ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera.

Mwanamvua Mrindoko ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi na Stephen Kagaigai ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na kabla ya uteuzi huo alikuwa Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na anachukua nafasi Anna Mghwira ambaye amestaafu.

Wengine walioteuliwa ni Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kuchukua nafasi ya Christine Mndeme ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Omary Mgumba anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe kuchukua nafasi ya Brigedia Jenerali Nicodemus Mwangela ambaye amestaafu na Makongoro Nyerere yeye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara.

Thobias Andengenye yeye anaendelea kuwa mkuu wa mkoa wa Kigoma na Marwa Rubirya naye anaendelea kuwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe.

Uteuzi wa viongozi hao unaanza leo na wataapishwa tarehe 18 mwezi huu saa 9:00 alasiri, Ikulu jijini Dar es salaam.