Raia wa kigeni watakiwa kuondoka kwenye machimbo

0
308

Serikali ya Nigeria  imeagiza raia wa kigeni kuondoka katika machimbo ya madini yaliyopo kwenye jimbo la Zamfara ndani ya kipindi cha saa 48.

Agizo hilo limetolewa na Ikulu ya Nigeria kwa madai kuwa raia hao wa kigeni wamekua chanzo cha vitendo vya wizi pamoja na vile vya utekaji nyara.

Katika taarifa yake, Ikulu ya Nigeria pia imeagiza kusitishwa haraka iwezekanavyo kwa shughuli zote za uchimbaji wa madini katika jimbo hilo la Zamfara na kwenye majimbo mengine yaliyoathiriwa na  vitendo hivyo vya wizi na utekaji nyara.

Wamiliki wote wa Kampuni za uchimbaji madini watakaokaidi agizo hilo wameonywa  kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kufutiwa leseni zao.

Hivi karibuni, mamia ya Wakazi wa  jimbo la Zamfara  waliandamana katika mitaa mbalimbali ya mji mkuu wa Nigeria, – Abuja kwa lengo la kumshinikiza Rais Muhammadu Buhari wa nchi hiyo kutafuta njia ya kukabiliana na vitendo vya uhalifu katika jimbo hilo, vitendo vilivyosababisha vifo vya watu wengi katika kipindi cha kuanzia mwaka huu hadi hivi sasa.

Zamfara  ni jimbo lenye utajiri mkubwa wa madini mbalimbali ikiwa ni pamoja na dhahabu, hali inayochangia kuwepo kwa vitendo vya wizi na utekaji nyara, na watu wanaofanya vitendo hivyo wamekua wakikimbilia nchi za jirani za Niger na Togo.